OSWALD KAHURUZI NA PASCAL MOMBO BAADA
YA KUTWAA MEDALI ROTARY HALF MARATHON 2014
Wanariadha 9 wa Klabu ya Riadha ya
Holili Youth (HYAC) wamejinasibu kufanya vizuri katika mbio zijazo za Rock City
Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu Jijini Mwanza.
Wanariadha hao walioko katika kambi ya
klabu hiyo katika kijiji cha Holili kilichopo kwenye miteremko ya mlima
Kilimanjaro kilometa 36 kutoka mjini Moshi ni Deo Hazard, Pascal Mombo,
Elibariki Buko, Lameck Misiwa, Alphonce Felix, Josephat Joswa Neema Mathias,
Adelina Audax na Lidwina Godfrey.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wanariadha hao walisema mbio hizo ni muhimu sana katika maandalizi ya mbio
nyingine kubwa zijazo hapo mwakani, kwani mazoezi wamefanya ya kutosha.
“Tumefanya mazoezi ya kutosha kuelekea
mbio hizo muhimu sana kwani zinatusaidia kwa maandalizi ya mbio zijazo kutokana
na kuwakutanisha wakali mbalimbali wa mbio ndani na nje ya nchi.” alisema
mwanariadha Deo Hazard
Kwa upande wake Kocha Timothy Kamili wa
klabu hiyo alisema wanariadha wake wanakimbia katika muda mzuri kwani kuna
michuano kadhaa ya hivi karibuni wamefukuza upepo kwa kiwango kinachotakiwa ni
suala la marekebisho madogo ili waweze kufanya vizuri.
“Wanariadha wetu (HYAC) wanakimbia kwa
kiwango cha kimataifa hivyo michuano kama hii inawaandaa zaidi katika mbio
kubwa za mwakani ambazo tunaendelea kutafuta mialiko kwa ajili ya kuwapeleka
ili wakaingarishe klabu na Tanzania kwa ujumla wake.”
Aidha Mkurugenzi wa Holili Youth
Athletics Club, Domician Genandi alisema wanariadha wake watakimbia half
marathon (kilometa 21), corporate race (kilometa 5) ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya mbio zijazo ndani na nje ya nchi.
Genandi aliongeza kusema anaendelea
kuwainua vijana wenye vipaji vya riadha nchini akianzia kwenye mbio fupi
kuelekea mbio ndefu.
“Vipaji vya riadha vipo ni suala la
uungwaji mkono kutoka kwa wadau mbalimbali, nimeanza na mbio fupi ambazo ni
muhimu kwa ukuzaji wa vijana kuelekea mbio ndefu, tunaendelea kutafuta mialiko
ya mbio mbalimbali nje ya nchi ili kuwapa uzoefu wanariadha wetu kwa manufaa ya
taifa kwa ujumla.”
Mwanza Rock City Marathon zilizinduliwa
mwezi Septemba mwaka huu na Rais wa Baraza la Michezo nchini (BMT) Dionis
Malinzi ambaye aliwataka waandaji ambao ni Capital Plus International (CPI)
kuendelea kuandaa mashindano hayo licha ya changamoto lukuki za riadha nchini.
Mbio hizo zitakazoanza katika Uwanja wa
Kirumba na kumalizikia uwanjani humo zimedhaminiwa na taasisi mbalimbali
zikiwemo NSSF, TSN Group Ltd, Bodi ya Utalii nchini (TTB), Africa Barrick
Gold, Nyanza Bottlers, Mfuko wa Pensheni (PPF), Sahara Communications, Shirika
la Ndege nchini (ATCL), IPTL, TANAPA, New Mwanza Hotel na New Africa Hotel.
Rock City Marathon ilianza mwaka 2009
na kufanya kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kukuza utalii nchini
yanayofanyika kila mwishoni mwa mwaka katika Kanda ya Ziwa.