Wanariadha kutoka katika klabu
ya riadha ya Holili Youth (HYAC) wamejinasibu kufanya vizuri katika mbio za
Rotary Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 14 mwaka huu, Jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza Mkurugenzi wa HYAC,
Domician Genandi alisema wanariadha wake wana ari na shauku ya kufanya vizuri
baada ya kujinoa kwa muda mrefu katika kambi waliyojichimbia katika kijiji cha
Holili, wilayani Rombo.
“Mazoezi ya kutosha wamefanya
chini ya kocha Timothy Kamili, tunajiamini kuelekea mbio hizo ambapo tuna ari
ya kuibakisha rekodi safi ya mwaka uliopita klabuni hapo ambapo Alphonce Felix
alitwaa nafasi ya kwanza” alisema Domician.
Genandi aliongeza kusema mbio hizo ambazo zitakuwa za kilomita 21
(half Marathon) zitasaidia kukuza wanariadha wake kuelekea mbio ndefu (full
marathon) kutokana na ukweli kwamba Tanzania bado haijapata wakimbiaji wazuri
wa mbio ndefu.
Pia Mkurugenzi huyo aliwataja
wanariadha wanne ambao watajitupa katika mbio hizo kusaka taji la ushindi mwaka
huu kuwa ni Pascal Mombo, Elibariki Buko, Lameck Misiwa na mwanadada Furaha
Sambeke.
Hata hivyo aliweka bayana
kuhusu wanariadha wengine wanaonolewa katika klabu hiyo pekee hapa nchini kuwa
wanaendelea kuwapa mazoezi ya nguvu kwa
ajili ya mbio zijazo.
Aidha Domician aliwataka wadau
wa mchezo wa riadha nchini kujitokeza kuwekeza kwa wanariadha ili kuwepo na
ushindani ambao utakuwa chachu ya mafanikio pindi michuano ya kimataifa
inapokaribia.
“Tanzania ina wanariadha wengi
wazuri, lakini changamoto ipo katika uwekezaji haupo kwa wanariadha hao hali
inayodumuza vipaji hivyo, kwani mwanariadha akifanya mazoezi peke yake bila
makocha na waangalizi hawezi kufanya inavyostahili” alisema Domician.
No comments:
Post a Comment