Wanariadha Alphonce Felix na John
Leornad wa Holili Youth Athletics Club (HYAC) wamesafiri usiku wa kuamkia leo
kwa ndege kuelekea Christchurch nchini New Zealand kwa ajili ya maandalizi ya
Jumuiya ya Madola baadaye mwaka huu nchini Scotland.
Mwanariadha mwingine kutoka HYAC, Wambura
Lameck yupo njiani akiwa na wanariadha wengine 45 wanaoiwakilisha Tanzania kuelekea
nchini Ethiopi, Uturuki na China kwa
maandalizi ya michuano hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wachezaji wanaokwenda katika kambi za
kujinoa na Mashindano ya Jumuiya ya Madola ‘Commonwealth Games’ itakayofanyika
jijini Glasgow, Scotland, Julai mwaka huu kuitumia vizuri ili waweze kurejea
nchini na medali.
WAZIRI MEMBE AKIKABIDHI
BENDERA YA TANZANIA
|
Alisema kitendo cha wao kufanya vizuri
kitakuwa ni faraja kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye amekuwa mdau mkubwa wa
maendeleo ya michezo, amekuwa na kiu ya kuondoka madarakani akiona medali
zikitua nchini, hivyo waende wakitambua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya
Watanzania ambao wamechoka kuona wakirejea mikono mitupu.
Alisema endapo watafanya vema katika
michuano hiyo, wanaweza kujikuta wako katika maisha mengine, maana watageuka
mashujaa wa Tanzania.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la
Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, alisema wachezaji hao wanatakiwa kufanya
jitihada katika mafunzo yao, ili watakaposhiriki Jumuiya ya Madola warejee na
ushindi ili kuwavutia wadhamini kuwekeza katika michezo mingine nje ya soka
kama ilivyo sasa.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia
kuboresha mchezo huo na kuweza kuleta ushindi nchini badala ya kubakia kuwa
kama washiriki au watalii kama ilivyokuwa hapo awali.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC), Filbert Bayi, alisisitiza kuwa wachezaji wanaokwenda mafunzoni
katika nchi walizopangiwa, wanatakiwa kushiriki vilivyo katika mazoezi, kwani
hakuna mchezaji atakayekwenda Glasgow bila ya kuwa na kiwango stahiki.
Timu za riadha, ngumi, judo, kuogelea,
mpira wa meza na kunyanyua vitu vizito, ziliagwa jana, ambapo zitakwenda
kujinoa China, New Zealand, Uturuki na Ethiopia. Zitaanza kuondoka kuanzia
kesho na kundi la mwisho litaondoka Mei 4.
CHANZO: JAIZMELALEO/TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment