Alphonce Felix
Wanariadha Catherine
Lange, Alphonce Felix na Johnson Jabir wameng’ara katika mbio za Serengeti Marathon
2014 zilizofanyika mwishoni mwa juma mkoani Simiyu wakikimbia kilometa 21 na
Rhino Fun Run 5k huku wakenya wakiwataabisha watanzania katika mbio ndefu za
kilometa 42.
Catherine Lange kutoka
Jeshi la Magereza mkoani Arusha aliwapita kina dada wenzake katika mbio za
kilometa 21 akikimbia kwa saa 1:10.28 akifuatiwa na Failuna Abdi (saa 1:12.46)
na nafasi ya tatu ikishikwa na Mary Naali aliyefukuza upepo kwa saa 1:13.10
Alphonce Felix kutoka
klabu ya Riadha ya Holili Youth (HYAC) aliweka rekodi tamu ya kuvutia katika
mbio hizo tangu kuanza kwake mwaka 2012 alipokimbia kwa saa 1:00.40 akifuatiwa na
Michael Wambura kutoka Mwanza aliyejitupa kwa saa 1:00.58 huku Dickson Marwa
akivikwa nafasi ya tatu kwa saa 1:01.05
Katika mbio za
kilometa 5 mwanariadha na mwandishi
habari Johnson Jabir aliweka rekodi yake ya kwanza alipofukuza upepo kwa dakika
18:25.87 akifuatiwa na mkali wa kutoka Simiyu Jeremiah Kichuli aliyekimbiza
upepo kwa dakika 18:40.34 na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Nindilo Yusto aliyekimbia
kwa dakika 19:15.34
Kwa upande wa wanawake
mbio za 5K Rhino Fun Run alichukua nafasi ya kwanza mwanadada kutoka England
Hannah WakeField aliyekimbia kwa dakika 23:28.20 akifuatiwa na Helen Severino
kutoka Tanzania aliyefukuza upepo kwa dakika 24:06.57 na nafasi ya tatu ilichukuliwa
na mtanzania Masalu Lengwa aliyetumia dakika 24:07.00
Kwa upande wao raia
kutoka Kenya walionekana imara sana katika mbio za kilometa 42 walipowatupa
watanzania ambapo wanaume Abraham Too kutoka Nandi Rift Valley alitumia saa
2:07.02 ikiwa ni rekodi murua katika mbio za Serengeti Marathon tangu
kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita, akifuatiwa na Julius Kilimo aliyefukuza
upepo kwa saa 2:07.59
Nafasi ya tatu
ilichukuliwa na mkenya Duncan Kwemboi aliyekimbia kwa saa 2:08.41 akifuatiwa na
mtanzania pekee aliyechomoza katika tano bora Andrew Sambu kutoka Arusha
akiweka rekodi safi ya saa 2:08.51 na nafasi ya tano ilifungwa na mkenya George
Nyamori aliyetumia saa 2:11.49
Hata hivyo utabe huo
ulionekana kwa wanawake ambapo Beatrice Tepkoriruta aliwaburuta wanawake
wenzake akitumia saa 2:40.07 akifuatiwa na Lilian Cherimo aliyekimbia kwa saa
2:40.08 na nafasi ya tatu ikichukuliwa na mkenya mwingine Dorcas Chesan aliyefukuza
upepo kwa saa 2:43.40
Mtanzania pekee katika
tano bora alikuwa Fabiola William kutoka Singida aliyetimua vumbi kwa saa
2:48.15 akishika nafasi ya nne huku Banuelia Brighton kutoka Moshi, Kilimanjaro
akishika nafasi ya saba kwa saa 3:48.15
Klabu ya Riadha ya
Holili Youth (HYAC) iliwika zaidi katika mbio za kilometa 21 huku Pascal Mombo
kutoka klabuni hapo akiiwakilisha katika full marathon aliposhika nafasi ya 11
akitumia saa 2:26.58
Josephat Joshua alishika
nafasi ya sita katika half marathon kutoka HYAC akikimbia kwa saa 1:02.03,
Lameck Misiwa akishika nafasi ya kumi akitumia saa 1:02.55 na Deo Hazard akitumia
saa 1:03.17 na kushika nafasi ya 11.
Kwa upande wa wanawake kutoka
HYAC, Furaha Sabaya alitumia saa 1:19.44 akishika nafasi ya tano ya mbio za
kilometa 21, Adelina Audax alitumia saa 1:27.32 akishika nafasi ya nane huku Neema Mathias akishika nafasi ya 10
akifukuza upepo kwa saa 1:33.21
Mkoa wa Simiyu katika
kilometa 21 ulianza kuonekana katika
nafasi ya 14, Emmanuel John alipoung’arisha mkoa huo kwa kukimbia kwa saa
1:12.33 huku mwanadada Holo Makoye akichomoza katika nafasi ya 12 alipotumia
saa 1:40.48
Wakenya walioonekana
katika kumi bora ya kilometa 21 ya Serengeti Marathon 2014 ni Wilson Kibrop (saa 1:01.24) akishika
nafasi ya nne, Isaac Koech (saa 1:01.44) nafasi ya tano na Vincent Osoro (saa
1:02.16) aliyeshika nafasi ya saba.
Kwa upande wake mgeni wa
heshima katika mbio hizo Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe alisema
Serengeti Marathon imeifanya mikoa ya Mara na Simiyu kung’ara kwa namna
nyingine kimichezo kutokana na uwepo wa wanariadha kutoka mataifa mbalimbali
ambayo kwa mwaka huu yaliongeza kutoka matatu mwaka uliopita hadi saba England,
Scotland, Ireland, USA, Hispania, Nigeria na Kenya.
No comments:
Post a Comment