Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini Tanzania
(RT) Suleiman Nyambui ameitolea uvivu serikali na kuitaka iache kuwadanganya
watanzania kuhusu mchezo wa riadha ambao umekuwa ukizorota kwa kipindi kirefu
sasa.
Akizungumza katika mjadala wa
wazi “Riadha Hard Talk 2014” ulioandaliwa na Holili Youth Athletics Club na
kufanyika mjini Moshi Februari 9 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Moshi
Club.
Nyambui alisema kwa muda sasa
lawama zimekuwa zikiwaangukia chama cha riadha nchini kwamba hawawajibiki hata
chembe katika kuinua mchezo huo ambao umeipatia sifa Tanzania miaka ya 1960
hadi 1980.
Katibu huyo aliongeza kusema
kuwa miaka ya nyuma serikali ilikuwa bega kwa bega na wanariadha, hali ambayo
iliwahamasisha kwa kiasi kikubwa kuinua vipaji vya chipukizi waliokuwa wakisoma
shuleni na vyuoni.
“Hali imekuwa tofauti sasa
ukilinganisha na miaka ya nyuma wakati tukisoma kwani mwanariadha aliheshimiwa
na watu wote hususani viongozi wa serikali tofauti ilivyo sasa”. Alisema
Nyambui
Pia Nyambui alisema serikali
imeshindwa kusimamia tasnia ya riadha na imebakia kutoa lawama kwa chama cha
riadha nchini, kwani mpaka sasa imeanzisha kamati za michezo katika wilaya na mkoa
kwa ajili ya kusaidia michezo kwa karibu zaidi lakini hali imekuwa mbaya
kutokana na kamati hizo kuwajibika kwa mchezo wa soka pekee huku mingine
ikisahaulika.
Aidha Nyambui aliongeza kusema
hadi sasa wamejitahidi kupeleka mapendekezo kadhaa baina yao na serikali ili
waweze kukaa chini na kufikia suluhisho la namna ya kuinua riadha lakini
serikali haijajibu hali inayoonyesha kutotilia maanani.
Kwa upande wake Kocha wa Kwanza
wa riadha hapa nchini Tanzania kutambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani Samwel
Tupa alikazia katika mjadala huo kuwa serikali imejisahau sana katika mchezo wa
riadha kutokana na ukweli kwamba hata kuwaruhusu wanariadha wafanye mazoezi katika uwanja wa
Taifa limekuwa ni suala lisilokubalika.
Tupa aliongeza kusema uwanja wa
taifa wenye vifaa muhimu katika mchezo wa riadha hauna msaada katika kuwainua
wanariadha wa Tanzania kufanya vizuri kimataifa.
Kocha huyo alisema hivi sasa uwanjani hapo kuna baadhi ya alama
za riadha zimeanza kufutika kutokana na kutotumika na nyingine hata kufunikwa
na nyasi na udongo huku watu wakifurahia rangi ya uwanjani hapo.
“Riadha Hard Talk 2014”
iliandaliwa ikiwa na madhumuni ya kukusanya maoni ya nini kifanyike kuinua
mchezo wa riadha ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 tangu mchezo wa riadha
utambulike rasmi nchini Tanzania; ambapo washiriki 60 walihudhuria kati ya 100
walioalikwa.