MWANARIADHA
Alphonce Felix wa Klabu ya Holili kutoka mkoani Kilimanjaro, jana aliibuka
mshindi katika mbio za kilomita 10 maalumu kuukaribisha mwaka mpya
zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo
zilizoandaliwa na Klabu ya Nyro ya jijini Dar es Salaam, zilianzia viwanja vya
Karimjee na kupita barabara mbalimbali kisha kumalizikia viwanjani hapo na
kushirikisha wanariadha kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Alphonce,
alishinda kwa upande wa wanaume akitumia dakika 28:11.35 huku kwa wanawake
Jackline Sakilu wa JWTZ Arusha akishinda akitumia dakika 33:18.33.
Mshindi
wa pili kwa wanaume alikuwa ni Alia Daudi wa Arusha akitumia dakika 28:23.32
akifuatiwa na Ezekiel Ngimba wa Holili 28:30.98, wa nne Andrew Sambu pia wa
Holili dakika 28:41.30 na wa tano aliibuka Said Makula wa Arusha 28:47.81.
Nafasi
ya sita ilienda kwa John Leonard wa Holili aliyetumia dakika 28:50.36 na
kufuatiwa na Abubakar Hussein wa JWTZ Arusha (28:54.96) huku wa nane akiwa ni
Dickson Marwa wa Holili (28:56.55), wa tisa Nelson Priva wa Holili (28:58.10)
na kumi bora ikifungwa na Wambura Lameck pia kutoka Holili, akitumia dakika
29:28.85.
Kwa wanawake,
Sakilu alifuatiwa na Catherine Lange wa Magereza Arusha dakika 33:43.73, Mary
Naali wa African Ambassador Athletics Club (AAAC), Arusha (34:12.09) akikamata
nafasi ya tatu, wa nne Natalia Uwezo wa Arusha (34:55.99) huku wa tano akiibuka
Amina Mohamed dakika 38:21.72.
Mshindi
wa sita aliibuka Furaha Sambeki akitumia dakika 39:29.47 akifuatiwa na Neema
Mathias (39:46.8), Pendo Pamba (41:32.54) wote kutoka Holili huku nafasi ya
tisa ikikamatwa na Neema Kisuda wa Zanzibar dakika 45:34.19.
Kwa
upande wa walemavu, Shukuru Khalfan aliibuka mshindi akitumia dakika 38:15.08
akifuatiwa na Mathias Jollo (47:04.08) na wa tatu aliibuka John Stephano
(52:18.86) wote kutoka Dar es Salaam.
Akizungumza
baada ya washindi kuzawadiwa zawadi zao za vitita vya fedha, Mratibu wa mbio
hizo, Sarah Ramadhani, aliwapongeza wanariadha waliojitokeza kushiriki mbio
hizo huku akiwaonya baadhi ya makocha wanaowatumia kimapenzi wachezaji wa kike
kuacha tabia hiyo, kwani wanaua na kukimbiza vipaji vya wanariadha wengi wa
jinsia hiyo.
Mgeni
rasmi katika mbio hizo, Ofisa Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, Adolph Halii,
alimpongeza muandaaji na wadhamini kwa jitihada zao za kuendeleza mchezo wa
riadha mkoani Dar es Salaam.
Pia
alishauri mashindano kama hayo yasiishie Dar es Salaam tu, bali pia yapanue
wigo na kufika mikoa mbalimbali kwa maendeleo ya mchezo huo hapa nchini.
Chanzo:
TANZANIA DAIMA Februari 3, 2014
No comments:
Post a Comment