HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Monday, 10 February 2014

RIADHA HARD TALK 2014 YAFANYIKA MOSHI




KATIBU WA CHAMA CHA RIADHA TANZANIA (RT) SULEIMAN NYAMBUI AKISISITIZA JAMBO

MOSHI: (JAIZMELALEO) - Mjadala wa wazi kuhusu riadha nchini Tanzania “RIADHA HARD TALK 2014”  ulioandaliwa na Holili Youth Athletics Club (HYAC) ya mkoani Kilimanjaro umefanyika jana Februari 9, mwaka huu huku ikibainika wachezaji na makocha wamekuwa wakiilalamikia serikali na Chama cha Riadha (RT) kutokana na elimu zao kuwa za kiwango cha chini.
 





Akizungumza katika mjadala huo uliofanyika mjini Moshi, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema kwa takribani miongo miwili kumeibuka tabia ya watanzania wakiwemo makocha na wachezaji wa mchezo huo kuilalamikia serikali na RT kutowekeza vya kutosha katika riadha.

Nyambui alisema serikali imekuwa ikilalamikiwa kuwa haitaki kuwekeza katika mchezo wa riadha, wakati huo huo RT nayo ikilalamikiwa kwa kutosimama imara.

“Tuwe wakweli mbele za Mwenyezi Mungu na atutazame sasa, inakuwaje watanzania, makocha na wachezaji kulalamika kila kukuchapo kuhusu mchezo wa riadha lakini kinachoonekana uvivu wa kufikiri na kiwango cha elimu kuwa duni kwa watanzania ndio kimesababisha lawama kwa serikali na RT” alisema Nyambui.

Hata hivyo Nyambui aliwataka makocha na wachezaji kuacha kutupa lawama kwa serikali na RT kutokana na ukweli kwamba wengi wao hawataki kuongeza viwango vyao vya elimu hali inayosababisha wawe waoga katika kutoa maoni yao.

“ Ukiwa umesoma hautakuwa mwoga katika kutoa maoni yako mahali husika kwa hekima na busara, kama ni kocha utakuwa ukifundisha kwa weledi tofauti na ilivyo sasa ambapo makocha wenye sifa za kufundisha mchezo huo wapo wachache hata wengine kugeuka kuwa madebe matupu yaliapo upepo ukivuma” aliongeza Nyambui.

Saturday, 8 February 2014

“RIADHA HARD TALK 2014” DEBATE



Venue: Moshi Club                                                                     Date: Feb.9,2014
RATIBA YA MJADALA
NA.
MADA
MHUSIKA/WAHUSIKA
1.
MAANA YA RIADHA
RT
2.
HISTORIA FUPI YA RIADHA TANZANIA
RT
3.
MAFANIKIO YA RIADHA TANZANIA
RT
4.
CHANGAMOTO ZA RIADHA TANZANIA
WOTE
5.
SULUHISHO LA CHANGAMOTO
WOTE
6.
MENGINEYO
WOTE
7.
HITIMISHO
RT/HYAC




http://cazro2320.edublogs.org/files/2012/08/athletics-10f6mpo.jpg
Mjadala huu umeandaliwa na HOLILI YOUTH ATHLETICS CLUB (HYAC).

Friday, 7 February 2014

RAIS KIKWETE YAITE MAKAMPUNI KUWEKEZA KATIKA RIADHA



Miaka ya 1980, nchini Kenya wakati huo Rais wa nchi hiyo alikuwa ni Daniel Arap Moi ambaye alikuwa akitawala akipokea madaraka kutoka kwa Mtangulizi na Mwasisi wa Taifa hilo Jomo Kenyatta.
 
Alichokifanya Moi aliutazama mchezo wa riadha nchini mwake na kuona kwamba unahitaji kufanyiwa mabadiliko ya hali ya juu ili kuiwezesha nchi hiyo kufanya vizuri kimataifa.

Aliyaita makampuni mawili akayaambia yauwezeshe mchezo huo kupanda kwa kiasi kikubwa, makampuni hayo mara baada ya kupewa rai hiyo yalianza kazi mara moja na ndio Kenya unayoiona hii leo ikifanya vizuri katika mchezo huo.

Kumekuwa na ubishani kwamba siasa haitakiwi katika michezo kwani ikiingia itasababisha madhara makubwa na hata michezo yenyewe isifanikiwe.

Lakini leo nasema “Siasa ndio kila Kitu” lakini je inatekelezwaje katika medani ya michezo.

Tumekuwa tukipiga kelele kuhusu mchezo wa riadha katika nchi ya Tanzania tangu enzi za kina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengineo waliandika historiakatika riadha ya Tanzania.

Moi aliongea tu na makampuni mawili tu na mambo yakenda vizuri, sasa inashindikanaje kwetu Tanzania ambako hakika tumejaliwa kuwa na hazina ya kila kitu.

Tulichokosa katika riadha yetu  nimaamuzi ya kiongozi wetu mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa mwenye hadhi ya kimataifa  Jakaya Mrisho Kikwete.

Sio lazima mheshimiwa Rais useme na vyombo vya habari tuje ila ni muhimu ukiona vyema kuita vyombo vya habari, kubwa zaidi ni kuyaita makampuni nchini kuwekeza katika Riadha.

Mheshimiwa Rais, binafsi nakupenda sana kutokana na uwezo wako wa kuweza kushawishi katika mambo mbalimbali, sasa ningekuomba ufanye na hili na kama ujuavyo muda wako wa kukaa madaraka ndio huo unapunga mkono.

Nimemzungumzia Moi kwasababu katika riadha alithubutu kufanya licha ya udhaifu wake katika serikali wakati ule hadi alipotolewa na Mwai Kibaki kupitia NARC, wakenya wanamkumbuka kwa hilo.

Kwako Kikwete ni muhimu ukafanya hivyo licha ya kutuletea Kombe la Dunia, UEFA Champions League kuzuru nchini lakini kumbuka jambo moja kwamba riadha ndio mchezo pekee ulileta medali nchini Tanzania.

Napolean Hill katika kitabu chake cha “Think, and Grow Rich” anaandika  kwamba ukiweza kufikiria katika mwono sahihi, utajiri utakuja pasipo mashaka.

Robert Kiyosaki katika kitabu chake cha “Cashflow Quadrant”  anasema kuwekeza katika masuala fulani husababisha maendeleo katika jamii husika, lakini hiyo inawataka watu wanajua nini maana ya kuwepo ulimwenguni.

Haina haja ya maandamano kuja kwako ikulu kukushinikiza Mheshimiwa Rais kuongea na makampuni maana wewe ndio mpini wa Tanzania hakuna wa kuleta “fyoko fyoko” ukishasema, Baba Sema Basi!!!! Wanao wazalendo wa Tanzania tujivunie Utaifa wetu.

Imeandikwa na Johnson Jabir, Columnist

Wednesday, 5 February 2014

HYAC YATESA MBIO ZA NEW YEAR 2014 DAR


MWANARIADHA Alphonce Felix wa Klabu ya Holili kutoka mkoani Kilimanjaro, jana aliibuka mshindi katika mbio za kilomita 10 maalumu kuukaribisha mwaka mpya zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo zilizoandaliwa na Klabu ya Nyro ya jijini Dar es Salaam, zilianzia viwanja vya Karimjee na kupita barabara mbalimbali kisha kumalizikia viwanjani hapo na kushirikisha wanariadha kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Alphonce, alishinda kwa upande wa wanaume akitumia dakika 28:11.35 huku kwa wanawake Jackline Sakilu wa JWTZ Arusha akishinda akitumia dakika 33:18.33.

Mshindi wa pili kwa wanaume alikuwa ni Alia Daudi wa Arusha akitumia dakika 28:23.32 akifuatiwa na Ezekiel Ngimba wa Holili 28:30.98, wa nne Andrew Sambu pia wa Holili dakika 28:41.30 na wa tano aliibuka Said Makula wa Arusha 28:47.81.

Nafasi ya sita ilienda kwa John Leonard wa Holili aliyetumia dakika 28:50.36 na kufuatiwa na Abubakar Hussein wa JWTZ Arusha (28:54.96) huku wa nane akiwa ni Dickson Marwa wa Holili (28:56.55), wa tisa Nelson Priva wa Holili (28:58.10) na kumi bora ikifungwa na Wambura Lameck pia kutoka Holili, akitumia dakika 29:28.85.

Kwa wanawake, Sakilu alifuatiwa na Catherine Lange wa Magereza Arusha dakika 33:43.73, Mary Naali wa African Ambassador Athletics Club (AAAC), Arusha (34:12.09) akikamata nafasi ya tatu, wa nne Natalia Uwezo wa Arusha (34:55.99) huku wa tano akiibuka Amina Mohamed dakika 38:21.72.

Mshindi wa sita aliibuka Furaha Sambeki akitumia dakika 39:29.47 akifuatiwa na Neema Mathias (39:46.8), Pendo Pamba (41:32.54) wote kutoka Holili huku nafasi ya tisa ikikamatwa na Neema Kisuda wa Zanzibar dakika 45:34.19.

Kwa upande wa walemavu, Shukuru Khalfan aliibuka mshindi akitumia dakika 38:15.08 akifuatiwa na Mathias Jollo (47:04.08) na wa tatu aliibuka John Stephano (52:18.86) wote kutoka Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya washindi kuzawadiwa zawadi zao za vitita vya fedha, Mratibu wa mbio hizo, Sarah Ramadhani, aliwapongeza wanariadha waliojitokeza kushiriki mbio hizo huku akiwaonya baadhi ya makocha wanaowatumia kimapenzi wachezaji wa kike kuacha tabia hiyo, kwani wanaua na kukimbiza vipaji vya wanariadha wengi wa jinsia hiyo.

Mgeni rasmi katika mbio hizo, Ofisa Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, Adolph Halii, alimpongeza muandaaji na wadhamini kwa jitihada zao za kuendeleza mchezo wa riadha mkoani Dar es Salaam.

Pia alishauri mashindano kama hayo yasiishie Dar es Salaam tu, bali pia yapanue wigo na kufika mikoa mbalimbali kwa maendeleo ya mchezo huo hapa nchini.

Chanzo: TANZANIA DAIMA Februari 3, 2014