HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Tuesday 9 December 2014

DEO LAZARO AMNG'ATA FABIAN JOSEPH, UHURU MARATHON 2014



Mbio za Uhuru Marathon 2014 zimegeuka shubiri kwa mwanariadha mkongwe, Fabian Joseph baada ya kukumbana na mkasa wa kung'atwa kidole kama ilivyokuwa kwa beki wa Italia, Giorgio Cheillini ambaye aling'atwa bega na mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
DEO LAZARO, KATIKA PICHA MBILI TOFAUTI KUFUATIA TUKIO HILO

Katika mbio hizo zilizohitimishwa jana katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam, Fabian alikumbana na mkasa huo baada ya kumaliza mbio, na ndipo wakaanza kuzozana na mpinzani wake kutoka Mbulu, Deo Lazaro aliyechukua hatua ya kumng'ata kidole.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya tukio hilo, mratibu wa mbio hizo, Innocent Meleck, alisema kitendo kilichofanywa na Lazaro si cha kiungwana na kwamba hata kama walikuwa na ugomvi hapo kabla hakupaswa kufanya hivyo.

Alisema kutokana na kufanya hivyo, Lazaro alipelekwa Polisi, na Fabian aliyefanikiwa kumaliza mbio hizo akiwa wa kwanza alipelekwa hospitali ya Mwananyamala na kupata matibabu na baadaye kuruhusiwa.

Hata hivyo, kocha wa wanariadha hao ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema Lazaro alimng'ata Fabian kutokana na kuchanganyikiwa na hali ya hewa ya joto ya jijini Dar es Salaam.

"Deo hawezi kumng'ata Fabian hivi hivi, alichanganyikiwa na hali ya joto na kuanza kupigana na mwenzake na hivyo kumng'ata kidole. Kwa sasa (jana saa 10:00 alasiri) wote wapo Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kuangaliwa afya zao," alisema kocha huyo.

Katika fainali hizo kwa upande wa mbio za Marathon, Fabian ameshika nafasi ya kwanza baada ya kutumia muda 1:05:09, huku nafasi ya pili ikienda kwa Alphonce Felix aliyetumia saa1:05:15, nafasi ya tatu imekwenda kwa Elia Dandi ambaye alitumia 1:05:22, wakati ya nne imechukuliwa na Ezekiel Ngimba aliyetumia 1:06:25.

Katika mbio za kilomita tano wanawake, Marrium Salum alishika nafasi ya kwanza, akifuatiwa na Grace Jackson huku ya tatu ikienda kwa Adelina Trasims, wakati wanaume ni Muhamed Nyambui nafasi ya kwanza, ya pili ikienda kwa Peter Sinde na ya tatu ikiwa halali ya Hafidhi Hafaa.

No comments:

Post a Comment