HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Tuesday 18 March 2014

HYAC YAJITOSA UDHAMINI SOKOINE MINI MARATHON 2014



K
labu ya Holili Youth Athletics Club (HYAC) ya mjini Holili, mkoani Kilimanjaro, imejitosa kudhamini mbio za Sokoine Mini Marathon zinazotarajiwa kufanyika Aprili 12, mwaka huu katika Kijiji cha Monduli Juu, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.


Domician Genandi, 
Managing Director 
(HYAC).
Katika udhamini huo, HYAC imetoa sh milioni moja zitakazotumika kuchapisha namba (Bibs), 1,000 za utambulisho za wanariadha.

Akizungumza na vyombo vya habari Mkurugenzi wa HYAC, Domician Genandi, alisema kilichomsukuma kufanya hivyo ni moyo wa uanamichezo na kuongeza kuwa, kwa mwaka huu wamedhamiria kuongeza nguvu zote kuinua mchezo wa Riadha nchini.

“Nimeamua kusaidia nikiwa kama mdau, sababu lengo letu ni kuendeleza michezo Tanzania, sisi wadau tunatakiwa tuwe na mtazamo wa ushindi kama taifa na si ushindi wa klabu zetu binafsi tu, au wanariadha wetu tu, HYAC tunatambua jitihada binafsi zinazofanywa na waandaaji kumuenzi hayati Sokoine,” alisema Genandi.

Aidha, Genandi alisema kwa mwaka huu klabu yake inatarajiwa kushirikisha wanariadha wengi zaidi, ambako lengo lake ni kuhakikisha anaendeleza rekodi ya mwaka jana.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alitaka Sokoine Mini Marathon ifanyike siku moja kabla ya tukio ili wanariadha nao wapate muda wa kuhudhuria maadhimisho ya mkongwe huyo kisiasa hapa nchini hasa ikizingatiwa kwamba maadhimisho hubeba vitu vingi.

Pia Domician alitanabaisha siku moja kabla inainua uchumi wa eneo husika hivyo siku zinapokuwa chache hufanya uchumi kukua taratibu kutokana na ukweli kwamba maadhimisho hayo hukusanya washiriki wengi kila mwaka.
Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday alisema kwa udhamini huo HYAC inakuwa klabu ya kwanza ya riadha hapa nchini kudhamini mashindano yanayoandaliwa na wadau wengine wa riadha na kuongeza kuwa, katika hilo wameonesha kweli kwamba wana nia nzuri ya kuendeleza michezo hapa nchini hasa riadha.

No comments:

Post a Comment