HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Thursday 1 May 2014

ALPHONCE FELIX, WAMBURA LAMECK WAITWA TIMU YA TAIFA MAANDALIZI COMMONWEALTH



Wanariadha Alphonce Felix na John Leornad wa Holili Youth Athletics Club (HYAC) wamesafiri usiku wa kuamkia leo kwa ndege kuelekea Christchurch nchini New Zealand kwa ajili ya maandalizi ya Jumuiya ya Madola baadaye mwaka huu nchini Scotland.

ALPHONCE FELIX(673) KATIKA NGORONGORO MARATHON 2014
Mwanariadha mwingine kutoka HYAC, Wambura Lameck yupo njiani akiwa na wanariadha wengine 45 wanaoiwakilisha Tanzania kuelekea nchini Ethiopi, Uturuki na China  kwa maandalizi ya michuano hiyo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wachezaji wanaokwenda katika kambi za kujinoa na Mashindano ya Jumuiya ya Madola ‘Commonwealth Games’ itakayofanyika jijini Glasgow, Scotland, Julai mwaka huu kuitumia vizuri ili waweze kurejea nchini na medali.

WAZIRI MEMBE AKIKABIDHI BENDERA YA TANZANIA
Alisema kitendo cha wao kufanya vizuri kitakuwa ni faraja kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya michezo, amekuwa na kiu ya kuondoka madarakani akiona medali zikitua nchini, hivyo waende wakitambua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya Watanzania ambao wamechoka kuona wakirejea mikono mitupu.

Alisema endapo watafanya vema katika michuano hiyo, wanaweza kujikuta wako katika maisha mengine, maana watageuka mashujaa wa Tanzania.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, alisema wachezaji hao wanatakiwa kufanya jitihada katika mafunzo yao, ili watakaposhiriki Jumuiya ya Madola warejee na ushindi ili kuwavutia wadhamini kuwekeza katika michezo mingine nje ya soka kama ilivyo sasa.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mchezo huo na kuweza kuleta ushindi nchini badala ya kubakia kuwa kama washiriki au watalii kama ilivyokuwa hapo awali.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, alisisitiza kuwa wachezaji wanaokwenda mafunzoni katika nchi walizopangiwa, wanatakiwa kushiriki vilivyo katika mazoezi, kwani hakuna mchezaji atakayekwenda Glasgow bila ya kuwa na kiwango stahiki.

Timu za riadha, ngumi, judo, kuogelea, mpira wa meza na kunyanyua vitu vizito, ziliagwa jana, ambapo zitakwenda kujinoa China, New Zealand, Uturuki na Ethiopia. Zitaanza kuondoka kuanzia kesho na kundi la mwisho litaondoka Mei 4.

CHANZO: JAIZMELALEO/TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment