HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Tuesday 15 July 2014

ZANZIBAR PWANI YATISHA KISAHANI NA MKUKI MBIO ZA TAIFA DAR, FAILUNA NA MARWA WANG’ARA TENA



Wanariadha kutoka visiwani Zanzibar wameng’ara katika urushaji wa kisahani na mkuki katika mbio za taifa mwaka huu, zilizohitimishwa juzi Jijini Dar es Salaam, huku Failuna Abdi wa Arusha na Dickson Marwa wakiwika tena katika mita 10,000 na 5,000.

Tama Jaha (Mjini Magharibi), Semeni Salmin (Kusini Pemba), Hafsa Ally (Mjini Magharibi) na Khadija Hija Shukuru (Kusini Pemba) waliibuka washindi katika urushaji wa kisahani (discus), wakitupa kwa umbali wa mita 31.25, 27.29, 26.48 na 25.77 kwa upande wa wanawake.

Mkoa wa Dar es Salaam ulishika nafasi ya nne, ukiwakilishwa na Subira Peter aliyerusha kwa umbali wa mita 26.20

Nafasi ya sita ilishikiliwa na Theresia Kikanka (Tabora) aliyerusha kisahani kwa umbali wa mita 17.95 na nafasi ya saba iliwakilishwa na Holo Charles (Mara) akirusha kwa umbali wa mita 16.75

Kwa upande wa urushaji mkuki (javelin), wanawake Hafsa Ally (Mjini Magharibi) alishika nafasi ya kwanza akirusha kwa umbali wa mita 37.84, akifuatiwa na MwanaAmina Hassan (Tanga) mita 35.52, Tama Jaha (Mjini Magharibi) mita 35.90

Mkoa wa Pwani ulishika nafasi ya nne katika urushaji wa mkuki wanawake, ukiwakilishwa na Tumaini James (mita 33.90), mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya tano ukiwakilishwa na Theresia Kikanka (mita 31.20). 

Kwa upande wa wanaume, katika urushaji wa mkuki, mkoa wa Pwani uliongoza na kunyakua nafasi ya kwanza ukiwakilishwa na Sabas Daniel (mita 54.76).

Nafasi ya pili ilishikwa na Daniel Mollel (Arusha) akirusha mkuki kwa umbali wa mita 53.50, Gilia Shagembe kutoka Tabora alishika nafasi ya tatu kwa umbali wa mita 51.02

Mkoa wa Dar es Salaam ulishika nafasi ya nne ukiwakilishwa na Charles Ibrahim aliyerusha mkuki kwa umbali wa mita 50.47 huku Said Thomas wa Arusha akimaliza watano kwa umbali wa mita 49.81

Failuna Abdi na Dickson Marwa baada ya kung’ara katika siku ya kwanza wakifanya vizuri katika mita 5,000 na 10,000; jana wameibuka washindi katika siku ya mwisho ya mbio hizo za taifa.

Mwanariadha Failuna Abdi aliuwakilisha vilivyo mkoa wa Arusha akishika nafasi ya kwanza, baada ya kukimbia kwa muda wa dakika 33:32.80 mita 5,000.

Nafasi ya pili ilishikwa na Catherine Range (Arusha) akifukuza upepo kwa muda wa dakika 34:00.15 akifuatiwa na Magdalene Chrispine (Kagera) alikimbia kwa muda wa 36:17.53

Mkoa wa Kagera ulimaliza tena katika nafasi za nne na tano kwa tiketi ya wanariadha wake Furaha Sabaya (dk. 39:15.24) na Irene Chima (dk. 40:78.16).

Dickson Marwa aliwanyanyua mashabiki wa mkoa wa Mara, aking’ara tena katika mbio za mita 5,000 akitumia muda wa dk. 13:38.48 na kuwapiku Fabian Nelson (Kilimanjaro), Joseph Teofil (Arusha), Gabriel Gerald (Kilimanjaro) waliokimbia kwa muda wa dk. 13:39.58, 13:40.29 na 13:45.26

Mkoa wa Kagera katika mita 5,000 wanaume ulishika nafasi ya tano ukiwakilishwa na Paul Goti aliyekimbia kwa muda wa dakika 13:59.06 akimpita Josephat Joshua (Kilimanjaro), Shamba Kitime (Arusha), Joseph Sule (Arusha) wakikimbia kwa muda wa dk. 13:59.55, 14:02.16, na 14:05.04

Hata hivyo katika siku ya mwisho kulijitokeza dosari nyingine ambayo iliwakuta baadhi ya waamuzi walipojikuta wakishangilia wakati wanariadha wakichukuana katika mbio za uwanjani hapo hivyo kusababisha uchukuaji wa rekodi kuwa mgumu, nusura ngumi zichapwe baina yao na wanariadha.

Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui alipohojiwa kuhusu sakata hilo alijitetea kwamba kila kitu waliachiwa kamati ya maandalizi wakati yeye alipokuwa nchini New Zealand.

Aidha Nyambui aliongeza kusema baada ya dosari lukuki kujitokeza katika mbio hizo za taifa mwaka huu, watakaa kitako kufanya upembuzi yakinifu likiwemo suala la uzoefu alioupata nje ya nchi kwa miezi takribani miwili aliyokaa.

No comments:

Post a Comment