HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Wednesday, 20 August 2014

KONA YA PRO, JULAI 2014: B'E BRAZUCA NA JUMUIYA MADOLA ZASHANGAZA DUNIA



B’E
Katika kipengele hiki tutaangazia matukio makubwa yaliyotukia kwenye mwezi  Julai mwaka huu ambapo tumeshuhudia Kombe la Dunia nchini Brazil na Michuano ya Jumuiya Madola ikirindima jijini Glasgow nchini Scotland.

Kombe la Dunia 2014 Brazil
Lilianza Juni 12 kwa kutumia mpira uliopachikwa jina la Brazuca, kwa wenyeji Brazil kufungua dimba dhidi ya Croatia ambapo walishinda mabao 3-1, ikiwa ni mtanange wa kundi A. 

Marcelo Viera aliweka rekodi ya kuwa wa kwanza kufumania nyavu alipojifunga hivyo kuwa mchezaji wa kwanza tangu Kombe la Dunia lianzishwe mwaka 1930, kujifunga kwa timu mwenyeji.

Aidha katika Kombe hilo kulishuhudiwa bingwa mtetezi Hispania akipokea kichapo cha mabao 5-1 kutoka Uholanzi, kisha 2-0 kutoka Chile na kuondolewa licha ya kushinda 3-0 dhidi ya Australia.

Hata hivyo haikuishia hapo kichapo cha mabao 7-1 ilichopokea Brazil kutoka kwa Ujerumani katika Kombe hilo ndicho kilichoacha gumzo kubwa kwani haijawahi kutokea katika hatua ya nusu fainali.

Pia timu za barani Afrika ambazo ni Cameroon, Algeria, Ghana, Nigeria na Ivory Coast zilijitahidi kucheza mchezo wa kuvutia licha ya kutofika mbali.

Algeria na Nigeria ndizo pekee zilizonusa hatua ya 16 bora baada ya kutoka katika hatua ya makundi (32). Algeria ilipambana na Ujerumani wakati Nigeria ikitoana jasho na Ufaransa.

Fainali ilichezwa katika uga wa Maracana Jijini Rio De Janeiro kati ya Ujerumani na Argentina ambapo Ujerumani (Die Mannschafts) ikivunja rekodi kwa kulinyakua kwa mara ya kwanza kutoka ardhi ya Amerika ya Kusini kwa kuizaba Albicelestes kwa bao 1-0 lilifungwa katika dakika ya 114 na Mario Gotze akitokea benchi.

Kubwa zaidi Miroslav Klose (Ujerumani) alivunja rekodi kwa kuwa mfungaji mwenye mabao mengi ya Kombe la Dunia akifikisha 17 na kuvunja rekodi ya Ronaldo de Lima aliyefunga mabao 15.

Kiatu cha dhahabu kilikwenda kwa nyota kutoka Colombia, James Rodriguez aliyetupia mabao 6 katika michuano hiyo iliwanyima raha wabrazil wakimaliza kwa kichapo cha mabao 3-0 kutoka Uholanzi.

Michuano ya Jumuiya ya Madola, Glasgow-Scotland
Maajabu hutokea kwani shilingi ni ndogo inazama kwenye maji lakini meli ni kubwa haizami; michuano ya Jumuiya ya Madola ilianza siku 10 baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia nchini Brazil yaani Julai 23 katika Jiji la Glasgow nchini Scotland.

Michuano hii hushirikisha nchi ambazo zilitawaliwa na Mwingereza katika medani ya michezo, hivyo michezo mbalimbali huwepo katika michuano hiyo Judo, riadha, ngumi za ridhaa, kuogolea, mpira wa meza na kadhalika.

Tanzania imeambulia patupu katika michezo mitano iliyoenda kuwakilisha katika michuano hiyo huko ughaibuni, wakati nchi jirani ya Kenya imetwaa medali 25 huku England ikiongoza kwa kuwa na medali nyingi.

Michuano hiyo imefungwa Agosti 3, mwaka huu kukishuhudia vifijo na nderemo vikipigwa katika Jiji la Glasgow.

Mkimbiaji anayeshikilia rekodi ya dunia ya kasi Usain Bolt siku ya Jumamosi ya Agosti 2 alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za relay 4×400.

Bolt alimkung’uta Mwingereza Danny Talbot aliyemaliza wa pili akikimbia kwa sekunde 37.58 huku Talbot akimaliza kwa sekunde 38.02

Bolt anajiandaa na mbio za Diamond IAAF za Agosti 28 katika uga wa Lepzig ambako anatarajiwa kuwa tishio zaidi.

Huku Danny Talbot akijiweka katika matumaini makubwa ya kunyakua medali katika Michuano ya Ubingwa wa Ulaya itakayofanyika baadaye mwezi ujao.

Haya ni matukio makubwa mawili yaliyojiri mwezi Julai na kukonga nyoyo za mashabiki duniani.
Prepared by:
Jabir Johnson
Blogger & Photo Journalist
+255-(0)-768 096 793

No comments:

Post a Comment