HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Thursday 2 October 2014

HOLILI YAJIPANGA ROTARY MARATHON 2014



Wanariadha kutoka katika klabu ya riadha ya Holili Youth (HYAC) wamejinasibu kufanya vizuri katika mbio za Rotary Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 14 mwaka huu, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Mkurugenzi wa HYAC, Domician Genandi alisema wanariadha wake wana ari na shauku ya kufanya vizuri baada ya kujinoa kwa muda mrefu katika kambi waliyojichimbia katika kijiji cha Holili, wilayani Rombo.

“Mazoezi ya kutosha wamefanya chini ya kocha Timothy Kamili, tunajiamini kuelekea mbio hizo ambapo tuna ari ya kuibakisha rekodi safi ya mwaka uliopita klabuni hapo ambapo Alphonce Felix alitwaa nafasi ya kwanza” alisema Domician.

Genandi aliongeza kusema  mbio hizo ambazo zitakuwa za kilomita 21 (half Marathon) zitasaidia kukuza wanariadha wake kuelekea mbio ndefu (full marathon) kutokana na ukweli kwamba Tanzania bado haijapata wakimbiaji wazuri wa mbio ndefu.

Pia Mkurugenzi huyo aliwataja wanariadha wanne ambao watajitupa katika mbio hizo kusaka taji la ushindi mwaka huu kuwa ni Pascal Mombo, Elibariki Buko, Lameck Misiwa na mwanadada Furaha Sambeke.

Hata hivyo aliweka bayana kuhusu wanariadha wengine wanaonolewa katika klabu hiyo pekee hapa nchini kuwa wanaendelea kuwapa mazoezi ya nguvu  kwa ajili ya mbio zijazo.

Aidha Domician aliwataka wadau wa mchezo wa riadha nchini kujitokeza kuwekeza kwa wanariadha ili kuwepo na ushindani ambao utakuwa chachu ya mafanikio pindi michuano ya kimataifa inapokaribia.

“Tanzania ina wanariadha wengi wazuri, lakini changamoto ipo katika uwekezaji haupo kwa wanariadha hao hali inayodumuza vipaji hivyo, kwani mwanariadha akifanya mazoezi peke yake bila makocha na waangalizi hawezi kufanya inavyostahili” alisema Domician.

No comments:

Post a Comment