HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Wednesday 5 February 2014

HYAC YATESA MBIO ZA NEW YEAR 2014 DAR


MWANARIADHA Alphonce Felix wa Klabu ya Holili kutoka mkoani Kilimanjaro, jana aliibuka mshindi katika mbio za kilomita 10 maalumu kuukaribisha mwaka mpya zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo zilizoandaliwa na Klabu ya Nyro ya jijini Dar es Salaam, zilianzia viwanja vya Karimjee na kupita barabara mbalimbali kisha kumalizikia viwanjani hapo na kushirikisha wanariadha kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Alphonce, alishinda kwa upande wa wanaume akitumia dakika 28:11.35 huku kwa wanawake Jackline Sakilu wa JWTZ Arusha akishinda akitumia dakika 33:18.33.

Mshindi wa pili kwa wanaume alikuwa ni Alia Daudi wa Arusha akitumia dakika 28:23.32 akifuatiwa na Ezekiel Ngimba wa Holili 28:30.98, wa nne Andrew Sambu pia wa Holili dakika 28:41.30 na wa tano aliibuka Said Makula wa Arusha 28:47.81.

Nafasi ya sita ilienda kwa John Leonard wa Holili aliyetumia dakika 28:50.36 na kufuatiwa na Abubakar Hussein wa JWTZ Arusha (28:54.96) huku wa nane akiwa ni Dickson Marwa wa Holili (28:56.55), wa tisa Nelson Priva wa Holili (28:58.10) na kumi bora ikifungwa na Wambura Lameck pia kutoka Holili, akitumia dakika 29:28.85.

Kwa wanawake, Sakilu alifuatiwa na Catherine Lange wa Magereza Arusha dakika 33:43.73, Mary Naali wa African Ambassador Athletics Club (AAAC), Arusha (34:12.09) akikamata nafasi ya tatu, wa nne Natalia Uwezo wa Arusha (34:55.99) huku wa tano akiibuka Amina Mohamed dakika 38:21.72.

Mshindi wa sita aliibuka Furaha Sambeki akitumia dakika 39:29.47 akifuatiwa na Neema Mathias (39:46.8), Pendo Pamba (41:32.54) wote kutoka Holili huku nafasi ya tisa ikikamatwa na Neema Kisuda wa Zanzibar dakika 45:34.19.

Kwa upande wa walemavu, Shukuru Khalfan aliibuka mshindi akitumia dakika 38:15.08 akifuatiwa na Mathias Jollo (47:04.08) na wa tatu aliibuka John Stephano (52:18.86) wote kutoka Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya washindi kuzawadiwa zawadi zao za vitita vya fedha, Mratibu wa mbio hizo, Sarah Ramadhani, aliwapongeza wanariadha waliojitokeza kushiriki mbio hizo huku akiwaonya baadhi ya makocha wanaowatumia kimapenzi wachezaji wa kike kuacha tabia hiyo, kwani wanaua na kukimbiza vipaji vya wanariadha wengi wa jinsia hiyo.

Mgeni rasmi katika mbio hizo, Ofisa Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, Adolph Halii, alimpongeza muandaaji na wadhamini kwa jitihada zao za kuendeleza mchezo wa riadha mkoani Dar es Salaam.

Pia alishauri mashindano kama hayo yasiishie Dar es Salaam tu, bali pia yapanue wigo na kufika mikoa mbalimbali kwa maendeleo ya mchezo huo hapa nchini.

Chanzo: TANZANIA DAIMA Februari 3, 2014

No comments:

Post a Comment