HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Tuesday 11 February 2014

RT YAIUMBUA SERIKALI YA JK



Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini Tanzania (RT) Suleiman Nyambui ameitolea uvivu serikali na kuitaka iache kuwadanganya watanzania kuhusu mchezo wa riadha ambao umekuwa ukizorota kwa kipindi kirefu sasa.


Akizungumza katika mjadala wa wazi “Riadha Hard Talk 2014” ulioandaliwa na Holili Youth Athletics Club na kufanyika mjini Moshi Februari 9 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Moshi Club.

Nyambui alisema kwa muda sasa lawama zimekuwa zikiwaangukia chama cha riadha nchini kwamba hawawajibiki hata chembe katika kuinua mchezo huo ambao umeipatia sifa Tanzania miaka ya 1960 hadi 1980.

Katibu huyo aliongeza kusema kuwa miaka ya nyuma serikali ilikuwa bega kwa bega na wanariadha, hali ambayo iliwahamasisha kwa kiasi kikubwa kuinua vipaji vya chipukizi waliokuwa wakisoma shuleni na vyuoni.

“Hali imekuwa tofauti sasa ukilinganisha na miaka ya nyuma wakati tukisoma kwani mwanariadha aliheshimiwa na watu wote hususani viongozi wa serikali tofauti ilivyo sasa”. Alisema Nyambui

Pia Nyambui alisema serikali imeshindwa kusimamia tasnia ya riadha na imebakia kutoa lawama kwa chama cha riadha nchini, kwani mpaka sasa imeanzisha kamati za michezo katika wilaya na mkoa kwa ajili ya kusaidia michezo kwa karibu zaidi lakini hali imekuwa mbaya kutokana na kamati hizo kuwajibika kwa mchezo wa soka pekee huku mingine ikisahaulika.

Aidha Nyambui aliongeza kusema hadi sasa wamejitahidi kupeleka mapendekezo kadhaa baina yao na serikali ili waweze kukaa chini na kufikia suluhisho la namna ya kuinua riadha lakini serikali haijajibu hali inayoonyesha kutotilia maanani. 

Kwa upande wake Kocha wa Kwanza wa riadha hapa nchini Tanzania kutambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani Samwel Tupa alikazia katika mjadala huo kuwa serikali imejisahau sana katika mchezo wa riadha kutokana na ukweli kwamba hata kuwaruhusu  wanariadha wafanye mazoezi katika uwanja wa Taifa limekuwa ni suala lisilokubalika.

Tupa aliongeza kusema uwanja wa taifa wenye vifaa muhimu katika mchezo wa riadha hauna msaada katika kuwainua wanariadha wa Tanzania kufanya vizuri kimataifa.

Kocha huyo alisema  hivi sasa uwanjani hapo kuna baadhi ya alama za riadha zimeanza kufutika kutokana na kutotumika na nyingine hata kufunikwa na nyasi na udongo huku watu wakifurahia rangi ya uwanjani hapo.

“Riadha Hard Talk 2014” iliandaliwa ikiwa na madhumuni ya kukusanya maoni ya nini kifanyike kuinua mchezo wa riadha ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 tangu mchezo wa riadha utambulike rasmi nchini Tanzania; ambapo washiriki 60 walihudhuria kati ya 100 walioalikwa.

No comments:

Post a Comment