HYAC

Attack with Style, Defend with Heart

Monday 23 June 2014

KONA YA PRO: JUNI 2014, UNAWAKUMBUKA?



Leo katika kipengele hiki tutaangazia mwanariadha mkongwe nchini Tanzania  John Stephen Akhwari na Michuano ya Olimpiki nchini Mexico mwaka 1968.

JOHN STEPHEN AKHWARI
Mwanariadha wa zamani John Stephen Akhwari, alizaliwa mwaka 1938 Mbulu, Tanganyika sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akhwari ni mwanariadha wa mbio ndefu, ambapo mwaka 1968 aliiwakilisha Tanzania katika Michuano ya Olimpiki iliyofanyika Mexico City.

1968 Olympic Marathon
John Akhwari alipokuwa akishiriki Mexico City, alipata mshtuko wa misuli (ilisinyaa) kutokana na hali ya hewa ya huko iliyokuwa ya juu katika Jiji la Mexico.

Akhwari hakuwahi kupata mazoezi katika Uwanda wa Juu alipokuwa nchini Tanzania. Hadi kilometa 19 alikuwa mbele na wakimbiaji wengine na alikuwa katika kiwango kizuri cha kumfanya ashinde lakini haikuwa hivyo.

Baada ya kupata matatizo hayo alifungwa bandeji katika goti, katika jointi na begani. Hata hivyo aliendelea kukimbia, na kumaliza wa 57 na kuwa miongoni mwa waliomaliza mbio hizo za kilometa 42.

Walianza wanariadha 75, mshindi alikuwa Mamo Wolde kutoka nchini Ethiopia aliyekimbia kwa muda wa saa 2:20:26; Akhwari alimaliza kwa muda wa saa 3:25:27, wakati kukiwa na watu wachache, maelfu ya watu wakitawanyika uwanjani hapo, na jua likikaribia kuzama.

Warusha matangazo kwa njia ya runinga wakiwa tayari wameshaondoka, ndipo neno likatoka katika vipaza sauti na spika zake kuwa kuna mshiriki mmoja anakaribia kumaliza.

Alipomaliza mstari wa kumalizia kilometa 42, pongezi, vigelegele na bashasha kutoka kwa hadhira ndogo vilimpokea.

Baadaye aliweza kuhojiwa na vyombo vya habari, kilichomfanya aendelee kukimbia wakati akiwa na majeraha Akhwari alisema

“Nchi yangu haikunituma maili 5000 kuanza mbio, ilinituma maili 5,000 kumaliza mbio”.

Akhwari na Riadha
 
Kabla ya Mbio za Mexico City Olympics 1968, Akhwari alikuwa amepambana katika michuano mbalimbali. Alimaliza wa kwanza katika African Marathon Championships.
Pia Akhwari alishika nafasi ya 5 katika Michuano ya Jumuiya ya Madola 1970 akikimbia kwa muda wa saa 2:15:05. Mshindi wa michuano hiyo alikimbia kwa muda wa saa 2:09:28.

Mkongwe huyo katika Michuano ya Jumuiya ya Madola 1970 alikimbia mita 10,000 kwa muda wa dakika 28:44 akipitwa na mshindi wa kwanza kwa sekunde 30 tu.

Hakika John Stephen Akhwari alikuwa mwanariadha wa dunia kwa miaka ile ya 1960-1970.

Baada ya kustaafu Riadha

Akhwari aliishi miaka mingi kijijini na familia yake, akiwa na mke mmoja na watoto 6. Walikuwa wakilima mashamba kwa bidii zote hadi pale dunia ilipotambua mchango wake katika riadha.

Alitunukiwa Tuzo ya Taifa ya Ujasiri (National Hero Medal of Honor) mwaka 1983.
Pia aliamua kutumia jina lake kuanzisha taasisi inayoitwa John Stephen Athletic Foundation; taasisi iliyojikita katika kufundisha wanariadha katika michuano ya Olimpiki.

Mwaka 2000 alialikwa katika Michuano ya Olimpiki nchini Australia, pia alionekana katika maandalizi ya Michuano ya Olimpiki mwaka 2008 Jijini Beijing akiwa kama Balozi wa kujitolea.

Aprili 13, 2008 alikuwa miongoni wa waliokimbiza Mwenge wa Olimpiki Jijini Dar es Salaam aliyeiwakilisha Tanzania nchini hapa.

Holili Youth Athletics Club (HYAC) ilikutana naye Desemba 22, 2013 katika Tamasha la Michezo la Karatu (Karatu Sports Festival) lililofanyika Karatu mkoani Arusha.

ILIYOPITA BOFYA KIUNGO HIKI

Imetayarishwa na:
Jabir Johnson, Afisa Habari na Mawasiliano
Holili Youth Athletics Club (HYAC)
Mei 2014.

No comments:

Post a Comment